Tuesday 12 March 2013

Taarifa ya Ufunguzi wa Kituo cha Watoto cha KANAANI – Kisongo Tar. 17 Feb 2013



Kituo cha Watoto cha Kanaani – Kisongo, kilifunguliwa rasmi na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Josaphat Lebulu kwa Misa Takatifu ya kukibariki siku ya Jumapili Tar. 17 Februari 2013. Misa hii ambayo iliadhimishwa na Mhashamu Baba Askofu Mkuu akishirikiana na mapadre  12 ilihudhuriwa na wana Familia ya Mungu ya Arusha zaidi ya 600, pamoja na marafiki wa kituo kutoka Ujerumani (Partnership for Africa), na viongozi wa serikali wakiwakilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa.

Kubarikiwa kwa kituo hiki ambacho ni mahsusi kwa ajili ya kulea watoto yatima na walio katika mazingira magumu, ni moja ya matukio makuu ya adhimisho la Jubilee Kuu ya Jimbo Kuu la Arusha. Jimbo letu linapoadhimisha miaka 50 ya uinjilishaji, kituo hiki ni moja ya alama mathubuti za ukomavu wa imani katika matendo. Kwa njia ya kituo hiki Wakristo wa Arusha watauonyesha upendo wa Kristo kwa kuwahudumia walio wahitaji sawa sawa na matakwa ya Kristo Mwenyewe (Math. 25: 32-46).

Kwa sababu hiyo, kituo hiki kimezinduliwa mwanzoni kabisa mwa kipindi cha Kwaresma, ikiwa ni alama ya kuungana na Kristo aliyeteseka kwa ajili yetu ili kutupatia uzima. Sisi nasi tunaalikwa kushiriki mateso ya Kristo kwa kujinyima ili tuwapatie watoto wa Kanaani uzima. Vivyo hivyo Kituo hiki kimejengwa kwenye lango la kuingilia Kituo cha Hija cha Kanaani, ili kwamba wote wanaokwenda hija ili kukutana na Kristo kule Kanaani, wakutane kwanza na Kristo katika nyuso za watoto hawa wahitaji.

Misa hii ya kubariki kituo hiki imekuwa ni ushuhuda wa uhakika wa utayari wa Familia ya Mungu hapa Arusha kumiliki kwa matendo kituo hiki. Ushuhuda huu umeonekana kwa njia ya mambo matatu. Kwanza katika kujitokeza kwa wingi kuhudhuria Misa hii, ingawa eneo la kituo haliko karibu sana na barabara. Kulikuwa na vitu 600 ambavyo vyote vilikaliwa na watu wengi wakakosa viti vya kukalia. Ni jambo la kuheshimu kwamba Mapadre pia ambao siku ya Jumapili ni vigumu kupata nafasi, waliwakilishwa vizuri na wenzao ambao waliweza kufika kwa idadi kubwa.

Pili ushuhuda huu ulionekana katika michango mbalimbali ambayo ilituolewa papo hapo na wana Familia ya Mungu. Pamoja na sadaka, jumla ya shilingi 4,690,800 taslimu zilichangwa siku hiyo. Pia kulikuwa na ahadi za michango zinazokadiriwa kuwa Shilingi 2,000,000. Pamoja na fedha, vitu mbali mbali vilitolewa kwa kusaidia watoto wa Kanaani kana inavyoanishwa katika jedwali hapa chini:

1.
Mafuta ya Kula
Kilogramu 117
2.
Sukari
Kilogramu 220
3
Mchele
Kilogramu 180
4.
Maharagwe
Kilogramu 40
5.
Unga wa Lishe
Kilogramu 36
6.
Mahindi
Kilogramu 60
7.
Maji ya Kunywa ya Chupa
Lita 46
8.
Unga wa Ugali
Kilogramu 70
9.
Majani ya Chai
Kilogramu 6
10.
Chumvi
Kilogramu 13
11.
Dawa za Meno
Paketi 20
12.
Mafuta ya Kupakaa
Katuni 4
13.
Madaftari
108
14.
Toilet Paper
Katuni 3
15.
Kalamu za wino
Boksi 1
16.
Peremende
Katuni 2
17.
Sabuni za mche
Vipande 158
18.
Sabuni za kuogea
36
19.
Sabuni ya maji
Lita 10
20.
Sabuni ya Unga
Kilogramu 20
21.
Kiwi ya viatu
Kopo 4
22.
Nguo za aina mbalimbali
Nyingi
23.
Midoli ya kuchezea watoto
Mingi

Tatu katika utayari wa kujitoa kuwa marafiki wa kudumu wa Watoto wa Kanaani. Tayari watu binafsi kadhaa na vikundi vichache vimejitokeza na kujaza fomu za kuwa marafiki wa kudumu wa Watoto wa Kanaani. Hawa wanakuwa marafiki wa kudumu kwa kuchangia kiasi kisichopungua TSh. 5,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miaka wanayotaka wenyewe.

Tunamshukuru Sana Mungu na wana Familia ya Mungu wa Arusha kwa majitoleo haya. Ni matumaini yetu kwamba watu na vikundi vingi zaidi vitaendelea kujitokeza kuwasaidia watoto wetu hawa kwa michango yao ya hiyari na kwa kuwa marafiki wa kudumu wa watoto wetu.

No comments:

Post a Comment