Kituo cha Watoto cha Kanaani – Kisongo,
kilifunguliwa rasmi na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Josaphat Lebulu kwa Misa
Takatifu ya kukibariki siku ya Jumapili Tar. 17 Februari 2013. Misa hii ambayo
iliadhimishwa na Mhashamu Baba Askofu Mkuu akishirikiana na mapadre 12 ilihudhuriwa na wana Familia ya Mungu ya
Arusha zaidi ya 600, pamoja na marafiki wa kituo kutoka Ujerumani (Partnership
for Africa), na viongozi wa serikali wakiwakilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa na
Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa.
Kubarikiwa kwa kituo hiki ambacho ni mahsusi kwa
ajili ya kulea watoto yatima na walio katika mazingira magumu, ni moja ya
matukio makuu ya adhimisho la Jubilee Kuu ya Jimbo Kuu la Arusha. Jimbo letu
linapoadhimisha miaka 50 ya uinjilishaji, kituo hiki ni moja ya alama mathubuti
za ukomavu wa imani katika matendo. Kwa njia ya kituo hiki Wakristo wa Arusha
watauonyesha upendo wa Kristo kwa kuwahudumia walio wahitaji sawa sawa na
matakwa ya Kristo Mwenyewe (Math. 25: 32-46).
Kwa sababu hiyo, kituo hiki kimezinduliwa
mwanzoni kabisa mwa kipindi cha Kwaresma, ikiwa ni alama ya kuungana na Kristo
aliyeteseka kwa ajili yetu ili kutupatia uzima. Sisi nasi tunaalikwa kushiriki
mateso ya Kristo kwa kujinyima ili tuwapatie watoto wa Kanaani uzima. Vivyo
hivyo Kituo hiki kimejengwa kwenye lango la kuingilia Kituo cha Hija cha
Kanaani, ili kwamba wote wanaokwenda hija ili kukutana na Kristo kule Kanaani,
wakutane kwanza na Kristo katika nyuso za watoto hawa wahitaji.
Misa hii ya kubariki kituo hiki imekuwa ni
ushuhuda wa uhakika wa utayari wa Familia ya Mungu hapa Arusha kumiliki kwa
matendo kituo hiki. Ushuhuda huu umeonekana kwa njia ya mambo matatu. Kwanza katika kujitokeza kwa wingi
kuhudhuria Misa hii, ingawa eneo la kituo haliko karibu sana na barabara.
Kulikuwa na vitu 600 ambavyo vyote vilikaliwa na watu wengi wakakosa viti vya
kukalia. Ni jambo la kuheshimu kwamba Mapadre pia ambao siku ya Jumapili ni
vigumu kupata nafasi, waliwakilishwa vizuri na wenzao ambao
waliweza kufika kwa idadi kubwa.
Pili
ushuhuda huu ulionekana katika michango mbalimbali ambayo ilituolewa papo hapo
na wana Familia ya Mungu. Pamoja na sadaka, jumla ya shilingi 4,690,800 taslimu
zilichangwa siku hiyo. Pia kulikuwa na ahadi za michango zinazokadiriwa kuwa
Shilingi 2,000,000. Pamoja na fedha, vitu mbali mbali vilitolewa kwa kusaidia
watoto wa Kanaani kana inavyoanishwa katika jedwali hapa chini:
1.
|
Mafuta ya Kula
|
Kilogramu 117
|
2.
|
Sukari
|
Kilogramu 220
|
3
|
Mchele
|
Kilogramu 180
|
4.
|
Maharagwe
|
Kilogramu 40
|
5.
|
Unga wa Lishe
|
Kilogramu 36
|
6.
|
Mahindi
|
Kilogramu 60
|
7.
|
Maji ya Kunywa ya Chupa
|
Lita 46
|
8.
|
Unga wa Ugali
|
Kilogramu 70
|
9.
|
Majani ya Chai
|
Kilogramu 6
|
10.
|
Chumvi
|
Kilogramu 13
|
11.
|
Dawa za Meno
|
Paketi 20
|
12.
|
Mafuta ya Kupakaa
|
Katuni 4
|
13.
|
Madaftari
|
108
|
14.
|
Toilet Paper
|
Katuni 3
|
15.
|
Kalamu za wino
|
Boksi 1
|
16.
|
Peremende
|
Katuni 2
|
17.
|
Sabuni za mche
|
Vipande 158
|
18.
|
Sabuni za kuogea
|
36
|
19.
|
Sabuni ya maji
|
Lita 10
|
20.
|
Sabuni ya Unga
|
Kilogramu 20
|
21.
|
Kiwi ya viatu
|
Kopo 4
|
22.
|
Nguo za aina mbalimbali
|
Nyingi
|
23.
|
Midoli ya kuchezea watoto
|
Mingi
|
Tatu katika
utayari wa kujitoa kuwa marafiki wa kudumu wa Watoto wa Kanaani. Tayari watu
binafsi kadhaa na vikundi vichache vimejitokeza na kujaza fomu za kuwa marafiki
wa kudumu wa Watoto wa Kanaani. Hawa wanakuwa marafiki wa kudumu kwa kuchangia
kiasi kisichopungua TSh. 5,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miaka wanayotaka
wenyewe.
Tunamshukuru
Sana Mungu na wana Familia ya Mungu wa Arusha kwa majitoleo haya. Ni
matumaini yetu kwamba watu na vikundi vingi zaidi vitaendelea kujitokeza
kuwasaidia watoto wetu hawa kwa michango yao ya hiyari na kwa kuwa marafiki wa
kudumu wa watoto wetu.
No comments:
Post a Comment